Monday, December 31, 2012

Bwana Daudi Arap Kimaiyo: Nawe Utayapindua Mawe Mangapi?



Printer-friendly versionPDF version
Sote tunakupongeza kwa dhati baada ya kuchaguliwa na kamati husika kuwa Mkuu Mpya wa Vikosi Vyote vya Jeshi La Polisi nchini mwetu, kama ilivyoratibiwa na Katiba yetu. Bila shaka unayafahamu majukumu yaliyo mbele yako hasa yanayohusu usalama wa wananchi na nchi, utendaji wa mageuzi makubwa katika jeshi la polisi ambalo tangu jadi, limepoteza na kukosa ladha na imani kutoka kwa wananchi wenyewe. Huduma wanazozipata wananchi wanapofika vituo vya polisi kutafuta usaidizi ni hafifu na duni.

Uzinduzi wa Mkuu wa Polisi ulianza lini na walikusudiwa kufanya yapi? Kwa kifupi, Mkuu wa Polisi ilianzishwa na serikali ya wabeberu, ikiongozwa na Malkia Elizabethi wa Pili, katika karne ya kumi na tisa ili kuwanyanyasa na kuwakandamiza Waafrika baada ya kunyakua makazi yao na kuwaweka vijijini. Diposa unapowataja Wakuu hawa wa Polisi nyakati hizo za ukoloni, babu na nyanya wanashikwa na hamasa na kigugumizi cha ajabu. Mtaje tu Brig.Gen F.S. Edward (1908-1922), F.D Thysen (1922-1925), R.C.A Cavendish (1931-1941), Kingsley-heath (1941-1943), Sandwich (1942-1947), na wengineo kama;Rorke (1950-1951); D.D.M Mcgoun (1951-1954); na aliyemkabidhi Bw Bernard Hinga, Mwafrika wa kwanza kuwa Mkuu wa Polisi nchini Kenya, Sir R. C Cutling (1955-1964).

Ni Wakuu hao wa polisi waliosababisha vifo na vitendo vingi vya jinai kwa Wakenya waliokuwa wakipigania uhuru wao kutoka kwa uvamizi wa nchi yetu kutoka kwa wakoloni. Si ajabu nikisema kwamba bw Kimaiyo una kibarua kigumu cha kufanya katika masuala mengi yanahusu usalama ambao sasa unayoitikisa taifa letu kila kunapokucha, mle vijijini na hasa mijini. Lakini swali ni hili: Je, nawe utayapindua pindua mawe mangapi kama ilivyokuwa awali kwa wale waliokutangulia? Utamtumikia na kumhudumia nani? Wakenya au wenye hadhi, wenye vyeo, wenye mali, wenye bila ...wananchi? Ni yapi tofauti utakayoyatenda ili kuihudumu taifa lako ipasavyo, bila uwoga wala mapendeleo? Utafuata maagizo ulopewa na katiba au yale yanatoka juu, kwa wao, kwa hao, kwa wale wale tu? Sifa zako za kutenda kazi zitatoka kwa wananchi au kwa wale waliojipachika juu mtini? Ni maswali kemkem tulio nayo kwako wewe Bw David Kimaiyo. Hata hivyo, Wakenya wana matumaini mengi kutoka kwako, hasa katika kugeuza na kuisafisha jeshi la polisi limeoza kimaadili, utendaji na utekelezaji wa kazi zao.

Kenya imewashuhudia na kutumikiwa na Wakuu wa Polisi takriban kumi tangu tulipojipatia uhuru hapo mwaka wa 1963. Nachukua fursa hii kuwataja mmoja mmoja ili wengi wafahamu tulikotoka na tunakoelekea. Mkuu wa kwanza wa Jeshi la Polisi punde baada ya kupata uhuru alikuwa Bw Bernard Hinga ambaye alihudumukati ya 1964-1978. Bw Hinga alifuatwa na Bw. Bethi (1978-1982); Bw Phillip Kilonzo ( 1988-1993); Bw Bw Shedrack Kiruki (1993-1996); Bw Duncan Wachira (1996-1998); Bw Philemon Abongo (1998-2002); Edwin Nyaseda (2002-2003); Meja Gen. Mohammed H. Ali (2004-2009) na mwisho, Bw Mathew Kirai Iteere. Kila mmoja wao alikuwa na jiwe alilojaribu kulisukuma likampigia nanga: likakosa kusukumika.

Katika huduma za Wakuu hao wa polisi, taifa letu liliyashuhudia majanga mengi ambayo hata siku ya leo, Wakenya hawajawahi kuambiwa ukweli wowote wa mambo. Mawe yakaporomoka kutoka milimani, yakatulia tuli. Wote hao wakatuahidi kuyapindua pindua mawe hayo kujua ukweli, ili kuwatuliza Wakenya walioshikwa na butaa. Mawe yakabadirika na kuwa magogo, hayapinduki hata. Yakaketi pwee! Bw Kimaiyo, waweza kuwa tofauti na wao. Tueleze uyatakayo kufanya. Katika kipindi hiki cha mabadiliko, hatutaki askari walionarenare. Tutakuunga mkono bila shaka.

Taaluma ulionayo baada ya kuhitimu ukuruta katika chuo maarufu cha Kiganjo na vyuo vingine na kujipatia shahada ya kupambana na wahalifu na uhalifu, yatuangazia matumaini mengi sisi tukiwa Wakenya. Tumia taaluma, ujuzi na ubusara wako kuwahudumia Wakenya bila kuyatazama makabila na wanakotoka.Kati ya yale ambayo wananchi wanayatarajia kutoka kwako ni:

a). Kutayarisha warsha kote nchini ili kubadirisha mawazo na fikra za jeshi la polisi kuhusu utoaji hudumu kwa wananchi.

b). Anzisha sera ambazo zitawapa maofisa wa polisi mashinani kuwafikisha wahalifu na wakiukaji wote wa sheria kizimbani bila kujali nyadhifa zao katika jamii.

c). Waelimishe askari kutoa na kuchukuwa hatua za dharura na haraka pale watoto, wanawake na wanaume wanatoa arifa kuhusu kupigwa, kunajisiwa, kujeruhiwa, navisa vingine vya kikatili, badala ya maofisa kuwauliza walalamishi wende wakasuluhishe hayo nyumbani.

d). Kutokomeza mara rushwa katika vikosi vyote vya polisi kwa kuimarisha mishahara yao, kuwapa makazi bora, kuwapa bima nzuri ya afya, kuimarisha uchukuzi wao wanapotoa hudumu za dharura, kuwapa vifaa hasa silaha za kisasa wanapopambana na wahalifu ambao wamepiga hatua kubwa katika kutanda uhalifu.

e). Kuwasambasa askari wa usalama sehemu zote nchini kwa kupunguza idadi ya askari wanaowalinda mawaziri, wake na watoto wao; Waziri mmoja kulindwa na karibu askari ishirini wakati askari mmoja anawahudumia Wakenya 600 sio haki, sio jambo la busara.

f). Kuziiga mbinu za marehemu Robert Shaw, ambaye kwa mkono mmoja tu, aliwaangamiza wahalifu maarufu kwa kufika katika eneo la uhalifu bila kuchelea.

g). Kuanzisha nambari moja maalumu na inayofanya kazi itakayotumia na Wakenya wote mahali popote walipo ili kutoa habari. Kuiomba mbunge kutunga sheria itakayolazimisha kampuni za simu kuweka kifaa katika simu kitakachoonyesha uhalifu uliporipotiwa.

h). Kuwatia moyo wananchi kushirikiana na poisi katika maeneo yao kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu miongoni mwao.

g). Kuwahimiza wananchi na viongozi kutii sheria bila shuruti, hasa kuchuchua sheria mikononi mwao kwa kuwateketeza washutumiwa wakati askari watazama tu..

h). Kuanzisha maabara ya upelelezi ambayo yatawanasa wahalifu kupitia alama za vidole, nyele, damu, mate, jasho, na kadharika kutoka eneo la uhalifu.

i). Kutaifisha bunduki zote haramu zilizo mikononi ya wahalifu na wananchi kwa kuweka sheria kali kwa wale watakaopatikana na silaha hizo.

j). Kumaliza ajali barabarani kwa kutekeleza sheria ipasavyo.

k). Kuimarisha kikosi cha upelelezi cha CID ambacho kimepoteza meno yote kikabaki kibogoyo.

l). Kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi ambao kwa miaka wamekuwa maadui, mahasimu.
Ukifanya hao, Bw Kimaiyo, utapunguza visa vya kuyapindua mawe yasiopinduka, kesi na upelelezi usiokuwa na mwisho, na visa vya kuwahudumia vigogo na wenye mali. Kumbuka umechaguliwa na katiba wala sio watawala kama ilivyo kwa waliokutangulia. Unapochaguliwa na katiba, unakuwa wewe ni mradi wa wananchi. Watakulinda wewe, liwe liwalo. Kanyaga barabara sasa, ni wakati wa kutumikia taifa lako, kwani, UTUMISHI NI KWA WOTE!!!!
By J. Mtulivu
The views expressed on this op-ed/blog are solely those of the author and do not reflect the opinions ofMwakilishi News Media, or any other individualorganization, or institution. The content on this op-ed/blog is not intended to malign any religion, ethnic group, club, organization, company, orindividual. The author himself is responsible for the content of the posts on this op-ed/blog, not any other organization or institution which he might be seen to represent. The author is not responsible, nor will he be held liable, for any statements made by others on this op-ed/blog in the op-ed blogcomments, nor the laws which they may break in this country or their own, through their comments’ content, implication, and intent. The author reserves the right to delete comments if and when necessary. The author is not responsible for the content or activities of any sites linked from this op-ed/blog. Unless otherwise indicated, all translations and other content on here are original works of the op-ed/blogauthor and the copyrights for those works belong to the author.
Original Author: 
J. Mtulivu

No comments:

Post a Comment